Skip to main content

MWAKYEMBE ASEMA AJARI ZA BARABARANI ZAITIA HASARA SERIKARI

 Ajali zaitia serikali hasara trilioni 3.2/- kwa mwaka mmoja



Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe pamoja na waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka wakipokea ripoti kutoka kwa kaimu katibu wizara ya mambo ya ndani, Augustine Shao

Serikali imepata hasara ya Sh. trilioni 3.2 kwa kipindi cha mwaka jana, kufuatia ajali za barabarani. Kamati ya kuchunguza matukio ya ajali za barabarani iliyoundwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, imebaini hasara hiyo katika uchunguzi wake.
Dk. Mwakyembe alisema hayo jana wakati akipokea Ripoti ya Kamati hiyo iliyopewa wiki mbili kuchunguza matukio ya ajali nchini.

Alisema kuwa kamati hiyo iliundwa Septemba 13, mkoani Dodoma na baada ya kumaliza kazi hiyo ilitakiwa kuwasilisha mapendekezo yake ili yaweze kufanyiwa kazi na kupunguza tatizo la ajali.

Alisema Kamati hiyo ina taarifa nzito zitakazofanyiwa kazi na miongoni mwa hayo ni hasara ya Sh. trilioni 3.2 iliyopata serikali kutokana na ajali za barabarani zilizotokea mwaka jana.

Alisema ataipitia ripoti hiyo yenye kurasa 60 kwa wiki moja na baada ya hapo atatoa taarifa kwa wananchi, lengo likiwa ni kubadilisha sekta ya uchukuzi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Augustino Shio, alisema baadhi ya vyanzo vya ajali walivyovigundua ni pamoja na kuwepo kwa makosa ya kibinadamu, madereva kunywa pombe na kupita barabarani bila kufuata sheria za barabarani na ubovu wa magari.

Alisema vifaa maalumu vya kupima kilevi vinaletwa ili dereva atakayebainika kutumia kilevi wakati akiendesha gari kuchukuliwa hatua kali ikiwamo kunyang’anywa leseni. Aliongeza kuwa baadhi ya madereva wanaendesha gari bila kuheshimu sheria za barabarani.

Kadhalika Kamati hiyo imependekeza mabasi kuwa na bima inayoeleweka ambayo itakuwa inatoa fidia kwa wahanga kwa kuwa watu wengi wakipata ajali wanatelekezwa na kujikuta wakiishi katika mazingira ya shida.

“Kuna mabasi yanatia aibu utakuta limenunuliwa kwa milioni 400 lakini bima yake inakatwa ya sh 80,000, hivyo jambo hilo linatakiwa kuangaliwa na tumependekeza wahanga wote wa ajali kulipwa na siyo kutelekezwa,” alisema

Aidha, alisema baadhi ya magari matairi yake yamechakaa na kuendelea kutembea barabarani jambo linalochangia kutokea kwa ajali.

Shio alisema Kamati hiyo ilibaini pia Mkuu wa Trafiki wa mkoa mmoja ambaye hata hivyo jina lake halikutajwa, kutoa leseni za daraja C kwa madereva wasio na ujuzi na walipofuatiliwa walibaini watu hao hawajaenda shule na leseni hizo zilitolewa kinyume cha sheria.

Shio alisema badala ya trafiki huyo kuchukuliwa hatua, alibadilishwa mkoa na kupelekwa mkoa mwingine huku akiendelea na cheo hicho hicho.

“Sasa najiuliza kilichofanyika ni nini wakati mkoani huko atakuwa akiendelea na mchezo huo huo wa kutoa leseni kwa watu wasio na elimu ya udereva,” alisema. 

chanzo NIPASHE 

Comments

Popular posts from this blog

NYOTA YA MZALIWA WA KWANZA

SANAA NI NINI?

STORY YA UTAKE